Taarifa Kuhusu Usaili wa walimu 2025 (Kada Za Ualimu)

Taarifa Kuhusu Usaili wa walimu 2025 (Kada Za Ualimu), Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilianzishwa kwa mujibu wa kifungu 29 (1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 iliyorejewa 2019, ambayo inaelekeza kuwepo kwa chombo maalumu cha kushughulikia mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma.

Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilitoa taarifa ya kusitishwa usaili wa Walimu tarehe 17 Oktoba, 2024 ambapo taarifa hiyo ilitokana na tangazo la kuitwa kwenye usaili la terehe 15 Oktoba, 2024.

Hivyo, kupitia tangazo hili, Katibu wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma anapenda kuwatangazia waombaji kazi wote wa Kada za Ualimu ambao usaili wao ulisitishwa kwa muda kuwa usaili huo utafanyika kuanzia terehe 14 Januari, 2025 mpaka tarehe 24 Februari, 2025. Ratiba ya usaili huu itapatikana katika Tovuti ya Sekretarieti ya Ajira (www.ajira.go.tz) na mitandao rasmi ya kijamii ya Taasisi.

Vile vile, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma anawajulisha wasailiwa wote wa kada za ualimu kuwa, usaili wa kuandika (mchujo) na mahojiano ya ana kwa ana utafanyika ndani ya mikoa wanayoishi wasailiwa na watapangiwa vituo vya kazi kulingana na ufaulu wao popote nchini.

Hivyo basi, waombaji kazi wa kada za ualimu na wale walioomba kwa ajili ya kada za amali na biashara mnatakiwa kuhuisha taarifa za makazi ya sasa (current physical address) kwenye mfumo wa ‘Ajira Portal’ ili muweze kupangiwa kituo cha kufanyia usaili jirani na maeneo mnayoishi kwa sasa.

Tangazo la majina kuonesha mtakapofanyia usaili litatolewa tarehe 06 Januari, 2025 kupitia tovuti ya Sekretarieti ya Ajira, mitandao rasmi ya kijamii ya Taasisi na akaunti za waombaji kazi kwenye mfumo wa ‘Ajira Portal’.

Vilevile wale wote walioitwa kwenye usaili wanatakiwa waje na vyeti vyao halisi vya taaluma, Cheti cha Kuzaliwa pamoja na kitambulisho halisi kwa ajili ya Utambuzi. Vitambulisho vinavyotambulika ni pamoja na; kitambulisho cha Uraia (NIDA), kitambulisho cha Mkazi, kitambulisho cha Mpiga kura, Hati ya Kusafiria, Leseni ya Udereva, Kitambulisho cha Kazi, Barua ya Utambulisho kutoka Ofisi ya Serikali ya Mtaa unaoishi au Sheha.

Aidha, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inawakumbusha watafuta fursa za ajira wote kuwa mchakato wa ajira unaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya Sifa, Haki, Usawa na Uwazi hivyo mnapaswa kujiepusha kutoa rushwa na kupokea taarifa potofu.

Lynn Chawala

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.

Makala Nyingine: