Matokeo Ya Uhakiki Waliochaguliwa Awamu Ya Pili 2024/2025 NACTVET Zamani ikijulikana kama NACTE,
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) linapenda kuutaarifu umma kuwa matokeo ya uhakiki wa awamu ya pili kwa waombaji waliochaguliwa kujiunga na programu mbalimbali kwa mkupuo wa Septemba 2024, katika ngazi ya Astashahada na Stashahada, yametolewa rasmi tarehe 7 Oktoba, 2024.
Jumla ya waombaji 45,540, ambapo kati yao wanawake ni 21,525 (47%) na wanaume ni 24,015 (53%), waliwasilishwa kwa ajili ya uhakiki kutoka katika vyuo vilivyokidhi vigezo vya kudahili wanafunzi. Kati ya hao, waombaji 44,088 (97%) walikidhi vigezo na sifa za kujiunga na programu walizochaguliwa, ambapo wanawake ni 20,722 na wanaume ni 23,366. Waombaji 1,452 (03%) hawakuwa na sifa katika programu walizochaguliwa.
Waombaji wote wanaweza kupata taarifa zao za uhakiki kwa kutumia msimbo uliotumwa kwenye namba zao za simu, kwa kubonyeza kitufe cha “Uhakiki Muhula wa Septemba 2024” katika tovuti ya Baraza www.nactvet.go.tz. Baraza linawasisitiza waombaji wote kutunza msimbo waliyotumiwa kwani ndio utakaotumika wakati wa usajili pindi mwombaji atakapofika chuoni kwa ajili ya kuanza masomo.
Aidha, Baraza linavielekeza vyuo kuhakikisha vinasajili waombaji waliohakikiwa na Baraza na kuonekana wana sifa. Usajili wa wanafunzi watakaofika vyuoni utaanza tarehe 10 Oktoba hadi 30 Novemba, 2024, na utafanyika kwa kutumia misimbo iliyotumwa na Baraza kwenye namba za simu za waombaji. Vyuo vitakavyokiuka taratibu za udahili, vitachukuliwa hatua stahiki.
Baraza pia litafungua dirisha la marekebisho kuanzia tarehe 10 hadi 15 Oktoba, 2024, ili waombaji waliohakikiwa na kuonekana hawakukidhi vigezo kwenye programu walizochaguliwa waweze kuomba programu wanazokidhi vigezo kupitia dirisha hilo. Aidha, vyuo vitumie nafasi hiyo kurekebisha taarifa za waombaji ambao taarifa zao hazijakamilika.
IMETOLEWA NA: Ofisi ya Katibu Mtendaji,
NACTVET
Tarehe: 7 Oktoba, 2024
Makala Nyingine:
Leave a Reply