TCU Kuongeza Muda Wa Udahili Kwa Mwaka Wa Masomo 2024/2025

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) inaufahamisha umma, Taasisi za Elimu ya Juu na wadau wa Elimu ya Juu ndani na nje ya nchi kuwa udahili katika awamu zote mbili kwa ngazi ya Shahada ya Kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu nchini kwa mwaka wa masomo 2024/2025 umekamilika. Majina ya waliodahiliwa katika Awamu ya Pili yatatangazwa na vyuo husika tarehe 05 Oktoba, 2024.

WAOMBAJI WALIODAHILIWA KATIKA CHUO ZAIDI YA KIMOJA

Waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja katika Awamu ya Pili na wale ambao hawakuweza kuthibitisha udahili katika Awamu ya Kwanza, wanapaswa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimojawapo kuanzia tarehe 05 hadi 21 Oktoba, 2024. Uthibitisho huo unafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri iliyotumwa kwa ujumbe mfupi kupitia namba zao za simu au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili.

Wale ambao hawatapata kwa wakati ujumbe huo, wanashauriwa kuingia kwenye mifumo ya udahili ya vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa ujumbe mfupi wenye namba maalum ya siri ili kuweza kujithibitisha katika chuo husika.

Aidha, uthibitisho wa udahili ufanyike kupitia akaunti ambayo muombaji alitumia wakati wa kuomba udahili. Kwa urahisi wa rejea, orodha ya majina ya waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja itapatikana kwenye tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz) tarehe 05 Oktoba, 2024.

KUFUNGULIWA KWA AWAMU YA TATU YA UDAHILI 2024/2025

Baada ya kukamilika kwa awamu zote mbili za udahili, Tume imepokea maombi ya kuongeza muda wa kutuma maombi ya udahili kutoka kwa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), baadhi ya waombaji ambao hawakufanikiwa kupata udahili katika awamu zilizopita na pia vyuo ambavyo bado vina nafasi vimeomba vipewe muda kuendelea kudahili.

Hivyo, Tume imeongeza muda wa udahili kwa kufungua Awamu ya Tatu na ya mwisho ya udahili itakayoanza tarehe 05 hadi 09 Oktoba, 2024. Tume inawaasa waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili au hawakuweza kupata nafasi ya kudahiliwa katika Awamu ya Pili kutokana na sababu mbalimbali, watumie fursa hii vizuri kwa kutuma maombi yao ya udahili kwenye vyuo wanavyovipenda.

Aidha, Tume inaelekeza Vyuo vya Elimu ya Juu nchini kuendelea kutangaza programu ambazo bado zina nafasi. Waombaji udahili na vyuo wanapaswa kuzingatia utaratibu wa udahili wa Awamu ya Tatu kama ilivyoainishwa katika Jedwali.

Jedwali: Utaratibu wa udahili katika Awamu ya Tatu kwa mwaka wa masomo 2024/2025

NA. TAREHE TUKIO
1 05 hadi 09 Oktoba, 2024 Kutuma maombi ya udahili katika Awamu ya Tatu.
2 13 hadi 15 Oktoba, 2024 Vyuo kuwasilisha Tume majina ya waliodahiliwa katika Awamu ya Tatu.
3 19 Oktoba, 2024 Vyuo kutangaza majina ya waliodahiliwa katika Awamu ya Tatu.
4 19 hadi 21 Oktoba, 2024 Kuthibitisha udahili kwa waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja katika Awamu ya Tatu na wale walioshindwa kuthibitisha udahili wao katika

awamu za udahili zilizopita.

WITO KWA WAOMBAJI UDAHILI

Waombaji udahili wa Shahada ya Kwanza wanakumbushwa kuwa masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha katika chuo kimoja yawasilishwe moja kwa moja kwenye vyuo husika. Kwa wale ambao watapata changamoto katika kujithibitisha, vyuo vyote vimeelekezwa kupokea taarifa zao na kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa.

Imetolewa na:

Prof. Charles D. Kihampa

KATIBU MTENDAJI

TUME YA VYUO VIKUU TANZANIA

Makala Nyingine: